Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Idara ya polisi katika eneo la Pwani imewaonya waganga wanaowahadaa na kudhulumu wananchi kukoma mara moja la sivyo wakabiliwe kisheria.

Akizungumza na wanahabari baada ya kuhudhuria mkutano wa kiusalama na maafisa wakuu wa idara hiyo mjini Mombasa siku ya Jumanne, Afisa mkuu wa polisi mjini Kilifi Joshua Ole Leina alisema kuwa waganga hao wamekuwa wakitumia mbinu za kuwalaghai wananchi.

Ole Leina alisema kuwa baadhi ya waganga hao wamekuwa wakiwashirikisha wananchi katika mambo ya kishirikina na kuwalaghai kwa kuwapa viapo ili kuwa wanachama wa kundi la MRC.

Leina alitaja maeneo ya Ganze, Chonyi na Matsangoni kama maeneo ambayo yako na idadi kubwa ya waganga.

“Tunawaonya waganga wote wale wanafanya biashara hiyo kukoma kuwalaghai wananchi na kuwapa mambo ya kishirikina na kuwashawishi kujiunga na vuguvugu la MRC. Serikali iko macho na itawakabili kisheria,” alisema Leina.

Aliongeza kuwa wananchi wamekuwa wakipoteza fedha nyingi kwa kulaghaiwa na waganga hao, huku wakiamini kuwa wanauwezo wa kuwapa baraka na mafanikio maishani mwao.