Polisi katika eneo la Tala, katika kaunti ndogo ya Matungulu, wamewakamata washukiwa wawili waliowapiga mawe chifu wa eneo hilo pamoja na polisi wa utawala, waliokuwa wanataka kuwakamata baada ya kupatikana wakitengeneza pombe haramu.
Akidhibitisha kisa hicho siku ya Alhamisi, OCPD wa Matungulu, Joseph Chesire alisema kuwa washukiwa hao, ambao ni wanaume wawili, walikuwa wakitengeneza pombe haramu katika kijiji cha Ikatine, pale chifu wa Tala, Pius Nzioka, akiwa na maafisa wa utawala walifika na kutaka kuwatia mbaroni.
Chesire alisema kuwa washukiwa hao walikaidi amri ya kusimama watiwe mbaroni na kuwashambulia maaskari hao kwa mawe.
“Washukiwa hao wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Tala, huku wakisubiri kufikishwa mahakamani kwa makosa ya kutengeneza pombe haramu na kuwashambulia maafisa wa polisi," alisema Chesire.