Share news tips with us here at Hivisasa

Mkuu wa polisi katika Kaunti ya Nyamira Rico Ngare amewaonya wahudumu wa magari dhidi ya kuendesha magari kwa kasi hasa wanapofika karibu na mashule na masoko ili kuepukana na visa vya ajali.

Haya yanajiri baada ya visa vya ajali vinavyoshuhudiwa karibu na mashule na masoko kuongezeka.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Alhamisi mjini Nyamira, mkuu huyo wa polisi aliwaomba madereva kuzingatia na kufuata sheria za barabarani wanapoendesha magari yao, kwani ukosefu wa kuzingatia sheria za barabarani ndio husababisha visa vya ajali kuongezka.

Ngare pia aliwaomba waendeshaji bodaboda kufuata na kuzingatia sheria za barabarani

“Naomba kila mhudumu wa uchukuzi katika kaunti ya Nyamira kuzingatia na kufuata sheria za barabarani ili kuepuka ajali na kupoteza maisha ya watu bila kutarajia,” alisema Ngare.

Aliongeza: “Katika siku za hivi majuzi, tumepoteza maisha ya watu hapa Nyamira kupitia ajali ambazo zinaweza kuepukwa. Jinsi wahudumu wa uchukuzi hufanya shughuli zao si halali.”

Ngare alisema kuwa wahudumu watakaopatikana wakivunja sheria za barabarani watakamatwa na kufikishwa mahakamani.