Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Afisa wa afya katika eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini, Kaunti ya Kisii, amewaomba wahudumu wa vichinjio na bucha kuzingatia usafi.

Akizungumza siku ya Alhamisi mjini Marani, alipokuwa akikagua nyama katika bucha mbalimbali za eneo hilo, Douglas Orora aliomba wahudumu wa vichinjio na bucha kuzingatia usafi ikiwa wanataka kuepa kuchukuliwa hatua ya kisheria.

Afisa huyo alisema wahudumu watakaopatikana wakiwauzia wakazi nyama ambayo imepimwa na kupatikana na kasoro watachukuliwa hatua kali za kisheria, kwa kuhatarisha maisha ya wananchi.

“Naomba wahudumu wa bucha na vichinjio kuzingatia usafi wanapowauzia raia nyama ili kuzuia wakazi kukumbwa na maradhi yanayosababishwa na uchafu,” alisema Orora.

Aliongeza, “Ikiwa nyama imepimwa na kupatikana na kasoro yoyote ambayo ni hatari kwa maisha ya binadamu, ni sharti nyama hiyo iziikwe kwenye shimo papo hapo kulingana na sheria ya afya nchini,” alisema Orora.

Wakati huo huo, afisa huyo aliomba wakazi kuwa macho na makini. Alisema iwapo wakazi watashuhudia kisa chochote ambacho ni kinyume na sheria za afya, wanapaswa kuwapasha maafisa wa afya ili wahudumu husika wachukuliwe hatua kali ya kisheria.