Wakaazi katika Kaunti ya Mombasa wameombwa kutowabagua watoto wa kike, na badala yake kuzingatia usawa wa jinsia ili kufanikisha malengo yao katika siku za usoni.
Akizungumza wakati wa kuadhimisha siku ya wanawake ulimwenguni siku ya Jumanne, Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko alisema kuwa lazima akina mama na wanaume katika jamii kuzingatia swala hilo la usawa wa jinsia ili kuwapa watoto wao elimu bora.
Kulingana na Mboko, swala la taasubi ya kiume umepitwa na wakati na kila mtoto nyumbani lazima achukuliwe kwa usawa kwani wana haki kikatiba kupata msingi bora wa elimu, na maswala mengine anayohitaji kwani demokrasia imechangiwa pakubwa na wanawake.
"Tafadhili wanawake tuzingatie usawa wa jinsia na kutowabagua watoto wa kike na kuhakikisha kuwa tunawatekelezea maswala muhimu sawa na watoto wa kiume, kwani wanawake nchini wamechangia pakubwa katika kuleta demokrasia,” alisema Mboko.
Wakati huo huo, aliwahimiza akina mama kutembelea afisi ya Wizara ya Vijana, Michezo na Jinsia katika Kaunti ya Mombasa kupata fumo za miradi ili kupata zabuni na kufanya miradi ya kimaendeleo na kujikumu kimaisha.