Wakaazi wa kaunti ya Nakuru wameraiwa kujitolea kutoa damu ili kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji damu katika hosipitali kuu ya mkoa ya Rift valley.
Naibu msimamizi wa kituo cha kutoa damu cha hosipitali kuu ya mkoa wa bonde la ufa Dismus Kimwa amesema kuwa hospitali nyingi katika kaunti ya Nakuru zimekabiliwa na uhaba wa damu.
Akizungumuza Jumapili katika hospitali ya Nakuru level five wakati waumini wa makanisa mbali mbali walipo shiriki shughuli ya kutoa damu, Kimwa alisema kuwa wakaazi wengi wa Nakuru hawajakumbatia swala la utoaji damu kwa hiari.
"Katika kaunti ya Nakuru tunakabiliwa na uhaba wa damu mara kwa mara na kuna baadhi ya wagonjwa hata hufariki kutokana na ukosefu wa damu," alisema Kimwa.
"Wakaazi wa Nakuru haswa vijana wanapaswa kuja na kutoa damu kwa hiari kwa kuwa hiyo damu huenda akawa ya manufaa kwa mtu wa karibu nawe," aliongeza Kimwa.
Kimwa alisema kuwa uhaba wa damu katika hosipitali hiyo pia unachangiwa na kuwa hosipitali hiyo inahudumia kaunti jirani za Baringo, Pokot Magharibi, Kericho.
Wakati wa shuguli hiyo zaidi ya watu 500 kutoka makanisa mbalimbali mjini Nakuru walitoa damu kwa hiari.