Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Chifu wa kata ya Sarang’ombe katika mtaa wa Kibera Danvas Mogire amewaonya wakaazi wa eneo hilo dhidi ya matapeli wanaojidai kwamba ni maejenti wa nyumba za kukodisha.

Mogire alisema kwamba visa vingi vimeripotiwa ambapo wakaazi wameibiwa pesa kwa njia za kilaghai na watu wanaowadanganya kwamba wanauwezo wa kuwasaidia kupata nyumba za kukodisha katika mtaa wa Kibera.

Akizungumza jumatatu alipoitisha kikao cha wanahabari afisini mwake, chifu huyo amewataka wenyeji kushirikiana na maafisa wa usalama na kuripoti visa vyovyote vya utapeli.

“Tumepata malalamishi kadhaa kwamba kuna wale wanawaibia wananchi wakiwadanganya kwamba ni maejenti wa nyumba. Kwa vile kuna ugumu wa kupata nyumba mtaani humu, wakaazi wengi hujipata mtegoni wanapokubali kutoa pesa kwa maatapeli hawa kama kodi,” alisema chifu huyo.

“Kuna kisa kimoja ambapo tulimwandama jamaa mmoja na kuhakikisha kwamba ameregesha pesa alizomhadaa mkaazi. Kwa hivyo yeyote atakaye tapeliwa ni vyema kuripoti hasa afisini mwangu ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wezi hao,” aliongeza.

Wakati huo huo, wamiliki wa nyumba wamehimizwa kufanya ukaguzi wa kutosha kabla ya kuwateua mawakala wanaosimamia nyumba zao. Kulingana na chifu huyo, hatua hii itasaidia kupunguza visa vya utapeli.

“Wamiliki wa nyumba ni vyema wachunguze kwa umakini wale wanaowafaanyia kazi kama maajenti ili kusaidia kukabiliana na matapeli,” Mogire alihimiza.