Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kamishna wa Kaunti ya Kisii Chege Mwangi ameomba jamii ya Gusii kutodhulumu mtoto wa kike hasa katika maswala ya masomo na uongozi.

Mwangi alisema kuwa watoto wa kike wanapaswa kupewa nafasi sawa ili kuendeleza jamii.

Kamishna huyo alisema ni wakati wa kufutilia mbali mila zisizo na msingi, na kuongeza kuwa hakuna haja ya kuwatenga watoto wa kike kwani jambo hilo huwazuia kunawiri maishani.

Akizungumza siku ya Alhamisi mjini Kisii, Mwangi aliwahimiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wa kike wanapewa nafasi sawa na wale wa kiume.

“Naomba jamii ya Gusii kutowatenga watoto wa kike. Wakazi wanapaswa kusahau mila za enzi za kale kwa sababu nchi yetu inaendelea kubadilika na kusonga mbele. Wototo wote wanapaswa kutumikiwa sawia katika masomo na uongozi,” alisema Mwangi.

Anayesimamia kitengo cha ukiukaji wa haki za kibinadamu katika kaunti hiyo Stella Achoki, alisema kutengwa na kudhulumiwa kwa watoto wa kike huchangia kwa kiasi kikubwa mtoto msichana kujiingiza katika mambo yasiyo ya kupedeza katika jamii.

Alisema kutengwa kwa wasichana sharti kukomeshwe ili kuzuia ndoa za mapema na wasichana kujiingiza katika mambo ya ukahaba na mambo mengine maovu.

“Naomba tuwajali watoto wa kiki kwa kuhakikisha kuwa wanapata fursa ya kupata elimu ili jamii yetu iendelee mbele,” alisema Achoki.