Vijana na wazee kutoka Kisii wameonywa dhidi ya uvutaji sigara ili kuzuia kuathiriwa na ugonjwa wa saratani.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumapili katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Kisii, Dkt Douglas Mariita anayesimamia ugonjwa wa saratani katika hospitali hiyo alisema uvutaji wa sigara unachangia pakubwa katika kuathiri wakazi na ugonjwa wa saratani.
Mariita alitoa wito kwa wazee na vijana kuasi uvutaji wa sigara ili kupunguza visa vya ugonjwa wa saratani nchini.
“Naomba wazee na vijana kutovuta sigara ili kuzuia kuathiriwa na saratani kwa kuwa ugongwa huo ndio husababisha vifo vingi ulimwenguni,” alisema Dkt Mariita.
Aidha, daktari huyo alisema pombe pia husababisha ugonjwa huo pamoja na ulaji wa nyama mara nyingi na kusema watu wanastahili kula nyama mara moja kwa wiki.
“Natoa wito kwa wananchi kupunguza ulaji wa nyama na kuasi utumizi wa pombe na sigara ili visa vya ugonjwa wa saratani viweze kupungua nchini,” alisema Dkt Mariita.