Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Afisa Mkuu wa Polisi Kisiwani Mombasa Martin Asin amesema wakazi wanaolenga kutumia fursa ya sherehe za Diwali, za Jamii ya Wahindi mjini Mombasa kuzua taharuki kuwa watakabilia kisheria.

Kulingana na Asin, waliyoruhusiwa kutumia fataki wakati wa sherehe hizo ni jamii ya wahindi pekee kulingana na taratibu za mila na tamaduni zao.

Asin alisema kwamba atakayepatikana akilipua fataki bila idhini ya maafisa wa polisi atatiwa nguvuni.

Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatano, Asin alisema kwamba sherehe hizo za Diwali zitafanyika siku ya Jumatano na jamii hiyo imetengewa kuidhinisha sherehe hizo katika maeneo ya uwanja wa Coast Jilcana mjini Mombasa.

Asin amewataka wakazi kutokuwa na hofu ya kiusalama wanaposikia milio ya fataki hizo zitakazolipuliwa na jamii hiyo wakati wa jioni huku akisema kwamba usalama umeimarishwa kisiwani Mombasa.

“Ninatoa onyo kali kwa wakazi waolenga kuzua taharuki katika sherehe za Diwali. Maafisa wa polisi wanashika doria na watawatia wakazi hao nguvuni kwa sababu wakilipua fataki kiholela watawatia wakazi hofu na sisi kama maafisa wa usalama haturuhusu hayo,” alisema Asin.

Sherehe hizo za Diwali huidhinishwa kila mwaka na jamii hiyo ya wahindi kulingana na taratibu za mila na tamaduni zao wakiadhimisha sherehe za mwaka mpya.