Wakazi katika eneo la Pwani wamehimziwa kushirikiana na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu ili kufahamu na kupigania haki zao.
Afisa wa nyanjani katika Shirika la kijamii la Kenya Community Support Centre alisema kuwa hatua hiyo itawawezesha wakazi kukabiliana na dhulma za kijinsia na unyanyasaji nchini.
Mwalimu Rama alisema kwamba iwapo kutakua na ushirikiano huo, basi taifa hili litakuwa na mabadiliko makubwa izingitiwa kuwa katiba inampa mwananchi uhuru wa kupigania haki zake.
Akiwahutubia wakazi mjini Mombasa siku ya Jumanne, Rama alisema kwamba kutokana na kukithiri kwa dhulma za kinjisia na unyanyasaji, pamoja na mauaji ya kiholela yanayotekelezwa nchini, ni sharti wakazi watambue haki zao.
"Sisi kama shirika tumejitolea kushirikiana na jamii kuhakikisha kwamba haki zao zinazingatiwa na dhulma zinazotekelezwa na baadhi ya viongozi kwa kuinyanyasa jamii zinasitishwa,” alisema Rama.
Afisa huyo wa nyanjani alisema kwamba tayari maafisa wa shirika hilo la kijamii wako mashinani kuihamasisha jamii kuhusu haki zao.