Wakuu wa idara katika Kaunti ya Kisii watafika mbele ya bunge la kaunti hiyo kueleza jinsi pesa za maendeleo katika bajeti ya mwaka wa 2014/2015 zilivyotumika.
Hii ni baada ya ripoti kuonyesha kuwa mamiolioni ya pesa tayari imetumika kufanya miradi ya maendeleo katika kaunti hiyo, huku wawakilishi wadi wakidai kwamba hawajaona miradi hiyo.
Mkuu wa idara ya fedha katika kaunti ya Kisii Kodek Omwancha, alifika mbele ya bunge la kaunti siku ya Jumatano wiki jana, ili kueleza jinsi pesa hizo zilivyotumika.
Omwancha alisema kuwa hawezi kueleza bayana jinsi pesa hizo zilivyotumika na kuwataka wakuu wa idara mbalimbali kufika mbele ya bunge hilo kueleza jinsi idara hizo zilivyotumia pesa hizo.
Wakuu hao wa idara wanatarajiwa kufika mbele ya bunge la kaunti siku ya Jumanne, ili kuelezea miradi ambayo kila idara imefanya na kiwango cha pesa kilichotumika.
Akizungumza siku ya Jumatatu na waandishi wa habari mjini Kisii, afisa anayesimamia utumizi wa pesa za serikali katika Kaunti ya Kisii, Ronald Oduso, alisema sharti wakuu hao wajitokeze na kusema yale kila idara imefanya na kiwango cha pesa kilichotumika.
“Wakuu wa idara watafika mbele ya bunge la Kaunti ya Kisii siku ya Jumanne ili kueleza jinsi kila wizara imetumia pesa kufanya maendeleo,” alisema Oduso.