Waziri wa elimu nchini Fred Matiang’i amewaomba walimu wote wakuu wa shule za upili nchini kutumia pesa wanazokabidhiwa na serikali kuu kwa njia inayofaa ili kuboresha viwango vya elimu.
Kulingana na waziri Matiangi, ambaye alizungumza mjini Nyamira, idadi kubwa ya walimu hao hawatumii pesa hizo vizuri kwa yale yanahitajika kama vile vitabu, bidhaa vya shule miongoni mwa vingine.
“Naomba walimu wakuu wote wa shule za upili kujaribu kila wawezalo kuhakikisha pesa wanazokabidhiwa na serikali ili kutoa elimu ya bure kwa wanafunzi zinatumika vizuri ili kuboresha viwango vya masomo,” alisema Matiang’i
“Ikiwa pesa hizo hazitumiki vizuri itakuwa vigumu viwango vya masomo kuinuka katika shule zetu, naomba sisi sote tuwajibike katika masomo, hakuna haja ya kuharibu mali ya serikali kwa kutotumia vizuri,” aliongeza Matiang’i
Wakati huo huo, Matiang’i aliomba walimu kutia bidii katika kuwafundisha wanafunzi ili kufanya vyema katika masomo.
Aidha, Matiangi aliwasuta wanasiasa ambao huingilia masuala ya elimu katika mashule mbalimbali, na kusema hilo huathiri masomo kwa shule.
“Naomba walimu wote kufanya kazi pamoja kuhakikisha viwango vya elimu vimeinuka kupitia motisha yenu kwa kufundisha wanafunzi,” alisisitiza Matiangi.