Share news tips with us here at Hivisasa

Wamiliki wa vilabu katika kaunti ndogo ya Matungulu wameonywa dhidi ya kuwauzia watoto walio chini ya umri wa miaka 18 vileo, hasaa msimu huu was krismasi.

Akizungumza katika Soko la Tala siku ya Jumanne, OCPD wa Matungulu Joseph Chesire alisema kuwa wakati wa sherehe za krismasi, watoto wengi hujihusisha na ulevi na matumizi ya dawa za kulevya.

Alisema kuwa watoto wengi wametiwa mbaroni na maafisa wa polisi kwa kupatikana katika vilabu.

Aidha, alielezea kuwa wenye vilabu na baa huwauzia watoto hao vileo bila kujua hatari iliyopo.

Vilevile, alisema kuwa hatua kali ya sheria itachukuliwa dhidi ya watakaopatikana wakiwauzia watoto vileo.

Akizungumzia swala la usalama, Chesire aliwahakikishia wenyeji kuwa usalama utaimarishwa msimu huu wa krismasi na kuwaomba kutokuwa na hofu.

"Japokuwa Matungulu kumekuwa na visa vingi vya ukosefu wa usalama, ningeomba wenyeji kutokuwa na hofu kwani usalama utaimarishwa ipasavyo," alisema Chesire.