Wanachama 42 wa Mombasa Republican Council (MRC) watajua hatma yao ya iwapo wataachiliwa kwa dhamana au la mnamo Januari 8, 2016.
Hakimu mkazi wa Mahakama ya Mombasa Paul Mutai, alisema siku ya Jumanne kwamba anahitaji muda zaidi kutathmini maelezo ya uchunguzi uliofanywa na maafisa waliowakamata wanachama hao kabla ya kuwapa dhamana.
Hii ni baada ya kiongozi wa mashtaka katika mahakama hiyo George Mungai, kumtaka hakimu kutowapa washukiwa hao dhamana kwa kusema ni tishio kwa usalama kwani washukiwa hao wamekuwa wakijishughulisha na usajili wa wanachama wapya kujiunga na kundi hilo.
Wakili wa washukiwa hao Yusuf Abubakar, alipinga hatua hiyo na kusema kuwa washukiwa wana haki kikatiba kupewa dhamana.
Hamadi Ramunda, mmoja wa washukiwa hao alisema kwamba walitiwa nguvuni na maafisa wa polisi katika makaazi ya mwenzao Hamadi Hassan, walipokuwa wakichangisha pesa za kusimamia kesi inayomkabili mwenyekiti wa baraza hilo Omar Mwamnuadzi.
Washukiwa hao walitiwa nguvuni mnamo Desemba 31, 2015 katika eneo la Tiwi huko Matuga, na wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kuandaa mkutano kinyume cha sheria, kuwa wanachama wa kundi lililopigwa marufuku pamoja na kuchangisha pesa za jumla ya shilingi elfu 67, 150 kinyume cha sheria.
Wote 42 wakiwemo wanawake sita wamekanusha madai hayo na kwa sasa wanazuiliwa rumande katika Gereza la Shimo la Tewa.