Wanaharakati wa maswala ya kijinsia wamelalamikia hatua ya kuonegezeka kwa dhuluma katika jamii eneo la Naivasha na viunga vyake.
Wakuu hao wamesema kuwa dhuluma hizo zimekuwa zikiongezeka huku wanawake wakiwa wale wanaolengwa kwa zaidi.
Esther Njeri, ambaye ni mmoja wa wanaharakati hao, amesema kuwa maeneo yanayopakana na ziwa la Naivasha yalikuwa yakiongoza huku kukiwa na kesi moja inayoripotiwa kila siku.
“Maeneo ya Karagita, kamere, Kongoni, Mai Mahiu na Kasarani yanaongoza kwa takwimu hizi,” alisema Njeri, ambaye pia ni Diwani mteule wa bunge la Kaunti ya Nakuru.
Aidha, kiongozi huyo amehoji kuwa kulikuwa na haja ya kuwaongezea machifu fedha ili kuweza kufika katika maeneo yote wanakosimamia.
Akizungumza Jumatatu na mwandishi huyu afisini mwake mjini Naivasha, Njeri alisema kuwa machifu wengi hawana magari au hata pikipiki, na iwapo watapewa vifaa hivyo, vita dhidi ya dhuluma hizo zitapungua.