Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi wa kisiasa wanaowachochea vijana kuzua vurugu katika eneo bunge la Malindi kunakotarajiwa kufanyika uchaguzi mdogo wameonya kuwa watakabiliwa kisheria na maafisa wa usalama.

Mshirikishi mkuu wa utawala ukanda wa Pwani Nelson Marwa amesema kuwa idara ya usalama imepokea ripoti za kijasusi kuwa baadhi ya wanasiasa wanawasajili vijana kutoka kaunti ya Mombasa, Kwale, Kilifi na Lamu ili kuzua vurugu na kutatiza uchaguzi huo mdogo.

Marwa alisema kuwa viongozi hao wanachunguzwa mienendo yao na lazima watiwe nguvuni na kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unakuwa wa huru na haki.

Marwa aliwaonya vijana kutokubali kutumiwa na viongozi hao akisema kuwa maafisa wa usalama watawakabili vikali vijana hao huku akiwataka maafisa wa usalama kuwa macho ili kuhakikisha kuwa uchaguzi huo haukumbwi na dosari.

"Tunawaonya viongozi wa kisiasa wanaowachochea vijana kuzua vurugu katika uchaguzi mdogo wa Malindi kuwa watakabiliwa kisheria. Kama serikali kamwe hatutaruhusu viongozi wazue taharuki miongoni mwa jamii,” alisema Marwa katika mkutano na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu.

Afisa huyo amewataka wanasiasa hao kufanya kampeni zao kwa amani na kujitenga na siasa za chuki na uchochezi ili kuzuia vurugu na uhasama wa kisiasa, huku akiwahakikisha wakazi kuwepo kwa usalama dhabiti.

Kauli ya Marwa inajiri huku mchakato wa kisiasa katika eneo bunge hilo la Malindi katika kaunti ya Kilifi ukionekana kuwa na ushindani mkali, kutokana na viongozi wa chama cha ODM na Jubilee wakiendelea sera za kuwapigia debe wagombea wao.