Wanawake wa Kaunti ya Mombasa wametoa wito kwa serikali kuongeza juhudi katika vita dhidi ya visa vya ubakaji, ambavyo walisema kuwa vinazidi kuongezeka katika eneo hilo.
Wakaazi hao walisema kuwa watoto wengi wamedhulumiwa lakini ni wachache sana wanaochukuliwa hatua za kisheria ipasavyo.
Akiongea na mwandishi huyu mjini Mombasa wakati wa sherehe za kuadhinisha siku ya wanamake duniani siku ya Jumanne, mwenyekiti wa maendeleo ya wanawake wadi ya Miritini Bi Halima Juma alisema kuwa hukumu inafaa kuongezwa dhidi ya wabakaji.
“Visa vya watoto kubakwa vinazidi kuongezeka katika Kaunti ya Mombasa hasa katika mtaa huu wa Miritini, wengi wa waathiriwa wakiwa watoto wadogo sana,” alisema Bi Halima.
Wanawake hao walisema mara nyingi washukiwa wa ubakaji wanapokamatwa, huachiliwa baada ya muda mfupi na kurudi mtaani, jambo wanalosema kuwa limechangia wengine kuona kwamba ni kitu cha kawaida.
“Mtu akikamatwa baada ya mwezi mmoja unashtukia yuko tena mtaani. Sasa hata tunashindwa ni sheria gani inatumika,” alisema Halima.
Mwenyekiti wa muungano huo tawi la Jomvu Bi Rehema Fuwe alisema kuwa serikali inafaa kuweka sheria kali kuliko zile zilizoko kwa sasa, ili kuhakikisha visa hivyo vinakomeshwa.
“Mimi nataka mtu akikamatwa asipewe hata faini ndio tuone kwamba tumefanikisha hili swala, kwa sababu bila ya kuchukua hatua hiyo, watoto wetu watazidi kudhulimiwa huku tukiona,” alisema Rehema.
Hata hivyo, akina mama hao waliishukuru serikali ya Kaunti ya Mombasa kwa kushirikiana na wananchi kuwahudumia watoto wanaobakwa.