Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mbunge wa Kitutu Masaba Timothy Bosire amewaomba wazazi katika eneo bunge lake kutafuta mbinu mwafaka za kusuluhisha tofauti zinazo zuka baina ya wazazi na usimamizi wa shule.

Akihutubu kwenye Shule ya msingi ya Kebuko siku ya Jumatano wakati wa kupokeza shule hiyo hundi ya shillingi elfu 500,000 kwa minajili ya ukarabati wa shule, Bosire alisema kuwa baadhi ya walimu wakuu wa shule, wamekuwa wakilalamikia upinzani wa wazazi kuhusiana na masuala muhimu ya maendeleo ya shule.

Alisema kuwa hali hiyo inafanya iwe vigumu kwa viwango vya elimu kuimarika.

"Ni jambo la kushangaza kwamba baadhi ya wazazi katika shule mbalimbali wamekuwa wakipinga usimamizi wa shule. Ni onyo langu kwa wazazi wa aina hiyo kwa kuwa sharti waheshimu walimu wakuu wa shule kwa maana wao ndio walio na mamlaka ya kuongoza shule hizo. Iwapo muna kitu mnachopinga, inafaa mtafute mbinu mwafaka badala ya kuwa na pingamizi," alisema Bosire.

Bosire aidha aliwataka wazazi kuwa na ushirikiano wa karibu na usimamizi wa shule mbalimbali ili kusaidia kuimarisha viwango vya elimu katika shule husika, akihoji kuwa ufitini hautasaidia kuimarisha elimu.

"Hii tabia ya wazazi ya kuingiza siasa shuleni kuhusiana na masuala fulani haifai kwa kuwa yafaa muwaheshimu walimu. Wao ndio viongozi wa shule na badala ya hayo, inastahii muwaunge mkono katika shughuli zao za kuimarisha viwango vya elimu," aliongezea Bosire.