Share news tips with us here at Hivisasa

Baadhi ya wazazi katika eneo la Kitutu Masaba wameitaka serikali kuruhusu shule kuwa na ratiba za vipindi vya masomo ya asubuhi, na pia kuruhusu kuwepo kwa masomo ya ziada wakati wa likizo ambayo yalikuwa yamepigwa marufuku.

Wazazi hao walisema kuwa hatua hiyo itakua njia mojawapo ya kuimarisha viwango vya elimu katika eneo hilo.

Wakihutubu kwenye Shule ya msingi ya Iranya siku ya Jumatano, wazazi hao wakiongozwa na msemaji wao Charles Anunda, walisema kuwa kwa muda sasa, shule nyingi kutoka eneo hilo zimekuwa zikifanya vibaya kwenye mitihani ya kitaifa, hali ambayo inastahili kurekebishwa.

"Hii sio mara ya kwanza kwa shule za eneo hili kufanya vibaya kwenye matokeo ya mtihani wa darasa la nane, KCPE. Tulifanya uchunguzi na kubaini kuwa walimu wengi hawamalizi silabasi kutokana na kutokuwepo kwa wakati unaofaa. Hiyo ndiyo sababu tunaitaka serikali kuruhusu wanafunzi kuwa na masomo ya likizo na hata pia kuwepo kwa darasani asubuhi ili wapata nafasi ya kumaliza silabasi," alisema Anunda.

Anunda aidha alisema kuwa iwapo masomo ya likizo yataanzishwa, huenda shule nyingi zikafanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa, akihoji kuwa matokeo ya mabaya hayafai kushuhudiwa tena.

"Tunaiomba serikali iruhusu kuwepo kwa masomo ya likizo kwa kuwa yataimarisha matokeo ya wanafunzi kwenye mitihani ya kitaifa.Hatutaki kuona shule zikifanya vibaya katika eneo hili,” alisema Anunda.