Mwanabiashara mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi mbili usiku wa kuamkia leo, Jumatatu, katika kituo cha kibiashara cha Bahati, Kaunti ya Nakuru na wezi ambao hawakuiba chochote kutoka kwa duka lake.
Hata hivyo, wezi hao waliiba duka lingine karibu na hilo kiasi cha pesa ambacho hakijulikani, na kisha kutoweka kwa miguu.
Inaarifiwa wezi hao wawili walienda katika duka la mwanabiashara huyo kabla ya kufunga kazi, ambapo mmoja wao alimwamrisha kuchukua mikono juu na kulala chini, lakini akaamua kumkabili ambapo mwizi wa pili alimpiga risasi.
Kulingana na wananchi, marehemu alifariki alipokuwa akipelekwa kwenye hospitali ya Maili Kumi.
Mwenyekiti wa wanabiashara hapo Bahati James Mwangi amelaani kitendo hicho, huku akiwataka polisi kushika doria haswa msimu huu wa sherehe.
“Kama wanabiashara hatuwezi kufanya biashara bila ya kuwepo na usalama, kwa hivyo msimu huu wa sherehe, polisi wazidishe doria za usiku,” alisema Mwangi.
Akiongea na mwandishi huyu, mwakilishi wa wadi hiyo Peter Nderitu, amesema inashangaza jinsi wahalifu hao walikuwa na ujasiri kwani kituo cha polisi kiko karibu na eneo la uhalifu huo.
“Kituo cha polisi wa AP, ofisi ya DC, Chifu na DO, kimo mita mia tatu kutoka pahali waliua mwanabiashara huyo. Ni kwa nini hawakuitikia wito huo kwa sababu wezi hao walitoweka kwa miguu?” alihoji Nderitu.
Polisi wanafanya uchunguzi kuhusu kisa hicho.