Share news tips with us here at Hivisasa

Rais Uhuru Kenyatta bado anaendelea na ziara yake katika eneo la Pwani, huku akiendelea kuzindua miradi mbalimbali pamoja na kukutana na viongozi wa eneo hilo kujadili mambo yanayowahusu Wapwani.

Hata hivyo, ziara ya rais ambayo kwa sasa imedumu kwa kipindi cha zaidi ya wiki tatu imeendelea kukumbana na masaibu mbalimbali huku baadhi ya viongozi wa upinzani wakiitaja kama mbinu ya kuwashawishi Wapwani kabla uchaguzi mkuu wa 2017, madai ambayo serikali ilipinga vikali.

Kisa cha hivi majuzi kilitokea siku ya Jumapili ambapo Rais Uhuru Kenyatta alizuru eneo la Malindi, Kaunti ya Kilifi.

Watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa ODM, waliweka bango lenye picha ya Gavana wa Kaunti ya Malindi Amason Kingi, pamoja na kiongozi wa Cord Raila Odinga lenye maandishi 'Karibu Malindi, Ngome Ya ODM.”

Hata hivyo, Rais Kenyatta hakupata fursa ya kuliona bango hilo kwani liliondolewa muda mfupi tu baada ya kuwekwa mahali hapo kutokana na kile kilichoonekana kama njia ya kumdhalilisha rais.

Tukio hilo limezua hisia tofauti sio tu eneo la Pwani, bali katika taifa nzima, kwani baadhi ya watu wameanza kuona wazi kwamba joto la kampeni za uchaguzi mkuu limeanza kujitokeza.

Baadhi ya wakaazi wa Mombasa walihusisha tukio hilo na uchaguzi mdogo wa ubunge unaotarajiwa kufanyika mjini Malindi.

“Saa hii kampeni za ubunge zinaendelea Malindi na sote tunajua hiyo ni ngome ya ODM. Mimi nahisi walikuwa wameweka bango hilo kama njia ya kumuonyesha rais kwamba Jubilee haiwezi kushinda kabisa,” alisema mkaazi mmoja.

Hapo awali, Rais Uhuru alisema kuwa yeye ni rais wa taifa na yuko na haki kutembea na kufanya kazi mahali popote nchini, licha ya kwamba wakaazi wanaunga mkono mirengo tofauti ya kisiasa.