Mbuga ya wanyama ya Shimba Hills inayoorodheshwa kama moja kati ya mbuga kubwa zaidi ukanda wa Pwani imetajwa kuimarika kiutalii katika siku za hivi karibuni.
Mbuga hiyo yenye aina mbalimbali za wanyama inapatikana katika eneo la Kwale na kwa muda mrefu imekuwa kivutio kikubwa cha watalii wa kigeni wanaopendelea kuzuru na kutazama wanyama.
Akiongea na wanahabari siku ya Jumatatu, afisa wa Shirika la wanyamapori nchini KWS Dadly Tsiganyiu alisema kuwa idadi ya watalii wanaozuru mbuga hiyo imeanza kuongezeka mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana.
“Tumekuwa na ongezeko la wageni tangu mwaka uanze tofauti na mwaka jana na hiyo imetufuraisha zaidi,” alisema Tsiganyiu.
Afisa huyo pia alisema kuwa wanategemea zaidi watalii kutoka mataifa ya kigeni na kuongeza kuwa idara ya utalii hupitia changamoto nyingi wakati mataifa hayo yanapotoa ithini ya wananchi wake kutosafiri Kenya kutokana na tishio za kiusalama.
Mbuga ya wanyama ya Shimbahills inapatikana kilomita 33 kutoka mji wa Mombasa ambapo watalii wanaotembelea mbuga hiyo hufurahia kutazama wanyama kama vile ndovu, pundamilia pamoja na manthari tulivu ya msitu.
Shimba Hills pia ndio mbuga ya kipekee nchini Kenya ambapo swara aina ya 'Sable Antelope' anapatikana.