Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi wa eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini kaunti ya Kisii wamemwomba mbunge wa eneo hilo Jimmy Nuru Angwenyi kuzinunulia shule za upili mabasi ya kuwasafirisha wanafunzi.

Wenyeji hao walisema shule nyingi hazina mabasi ya kuwasafirisha wanafunzi wao wanaposhiriki mambo mbalimbali yanayohusu masomo ya sekondari kama wakati wa michezo, uigizaji, muziki na pia kutizama uigizaji wa vitabu vya fasihi maarufu 'Set books'.

Wazazi katika eneo hilo walisema kuwa ukosefu huu wa mabasi hulazimisha wanafunzi kutumwa nyumbani kuleta pesa za kukodisha, jambo ambalo wakazi walisema hawalikubali.

Wakiongea na mwandishi huyu siku ya Jumapili katika eneo la Masakwe, wakaazi hao wakiongonzwa na Stanley Ombwori walimwomba mbunge wa eneo hilo kununulia mabasi baadhi ya shule hasa zile zinafanya vizuri katika mitihani ya kitaifa na pia michezoni.

Baadhi ya shule za upili ambazo walipendekeza zinunuliwe mabasi ni zile za Tambacha, Nyakeiri, Rioma, Nyagesenda, Marani na Nyakoora.

“Kuna shule za eneo hili ambazo zinafanya vizuri na zinastahili kununuliwa mabasi lakini hazina. Tunaomba Mbunge Angwenyi ajaribu awezalo azinunulie ili kurahisisha usafirishaji wa wanafunzi haswa katika michezo,” aliomba Godffrey Omariba mkaazi ambaye pia ni mzazi wa shule ya Nyakeiri.

Aidha , wakaazi hao walimwomba mbunge huyo kufadhili shule zinazofanya vizuri katika mitihani kama njia mojawapo ya kuwapa motisha wanafunzi.

“Kuna shule zingine ambazo wanafunzi wanafanya vizuri na wanastahili kufadhiliwa. Bado hakujakuwa na sherehe ya kuwatuza,” alisema Bi Rebbecah Onsarigo mkaazi na mzazi wa shule ya Tambacha.

Wakazi hao walidai kuwa shule katika maeneo bunge kwingineko hutuzwa na wanafunzi kuzawadiwa wakipita mitihani, jambo ambalo wamesema halijafanyika kwao.