Ongezeko la ukahaba katika mtaa wa Nyalenda, Kaunti ya Kisumu limekuwa kero kwa wengi wa wakazi huku jamii za eneo hilo zikitakiwa kuwapa wanao malezi yenye maadili.
Picha zinazonaswa mtani humo nyakati za usiku zinaonyesha wamama walio na umri wa makamo pamoja na wasichana wadogo wakiwa nusu uchi wakizurura mtaani kuwasaka wanaume.
Inakisiwa kuwa wamama na wasichana hao huuza mili yao ili kupata hela, hali ambayo wadadisi wanasema kuwa imechangia pakubwa ongezeko la ugonjwa wa ukimwi miongoni mwa jamii zinazoishi mjini Kisumu.
Douglas Pule ambaye ni mfanyibiashara wa hoteli na mkazi katika eneo hilo anasema kuwa, ''Huwa ni aibu sana ifikapo saa za jioni, wakati macho yako yanapoanza kuona watu wakike wakiwa nusu uchi wakipitapita mabele yako ukiwa pamoja na familia yako,'' alisema Pule katika mahojiano na Mwandishi huyu.
Aidha, mdokezi huyo alisema kuwa kero kubwa na baya sana ni kwamba wasichana wadogo wanaacha shule na kuingilia biashara hiyo haramu na hatari kwa maisha yao.
''Eneo hili limekuwa na idadi kubwa ya watoto wasichana wanaoacha shule wakijihusisha na ukahaba,'' alisema Pule.
Aidha, alidokeza kwamba hali hiyo huchangiwa na ukosefu wa maadili katika jamii pia ufukara ambapo mahitaji ya watoto hao hukosekana nyumbani na ndipo wanaamua kuanguka kwenye mtego huo.