Mwakilishi wa wadi ya Sensi iliyoko eneo bunge la Kitutu chache Kaskazini kaunti ya Kisii Ochong’a Nyagaka amewaomba wanasiasa kusubiri hadi mwaka wa 2017 kabla ya kuanza kampeni zao.
Mwakilishi huyo amesema kuwa wakati uliopo ni wa kufanya maendeleo akikariri kuwa viongonzi waliochaguliwa wanahitaji kupewa fursa ya kufanya maendeleo.
Akizungumza siku ya Jumanne katika mji wa Kisii mwakilishi huyo alisema wananchi wanahitaji maendeleo ila sio siasa kwani wakati wa siasa ulikamilika. Alisema kuwa mwaka wa 2017 utakapofika wagombeaji watakuwa na nafasi ya kuwaomba wakazi kura.
“Naomba wanasiasa waweke siasa kando ili tufanye maendeleo kwa wananchi , sisi viongonzi tunatimiza yale tuliwaahidi wananchi na wakati wa siasa utafika tu. Naomba wanasiasa kusubiri hadi wakati huo ufike,” Ochong’a alisema.
Wakati huo huo, mwakilishi huyo aliwaomba viongozi wote waliochaguliwa kufanya maendeo ili kutimiza yale waliyowaahidi wakazi wakati wa kampeni.
“Na wale waliochaguliwa kuwa viongonzi nawaomba wawe wanawafanyia maendeleo wananchi kila wakati ili kutimiza ndoto za maendeleo walizokuwa nazo wakati walikuwa wanatafuta kura,” alisisitiza.
Aidha, alisema siasa haziwanufaishi wakazi badala yake viongozi waungane na kuleta miradi ya kuimarisha hali ya maisha ya watu.