Walimu wakuu wa shule mbalimbali za upili katika Kaunti ya Kisii wameomba serikali ya kitaifa kutuma pesa kwa shule zao ili zitumike kununua kemikali ambazo wanafunzi wa kidato cha nne wanaoendelea kufanya mtihani wa kitaifa wa KCSE watatumia katika somo la chemia.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa serikali ya kitaifa hadi sasa haijatuma pesa zozote kwa shule za upili, jambo ambalo walimu wanahofia litaathiri matokeo ya somo hilo.
Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika mji wa Kisii, walimu hao wakuu wa shule za upili, wakiongozwa na mwenyekiti wao katika kaunti ya Kisii Jairus Ochoke walisema ikiwa serikali haitatuma pesa ifikapo siku ya Jumatano, basi huenda wanafunzi walazimike kuandika majina tu kwenye makaratasi yao ya mitihani na kuwasilisha makaratasi hayo bila kufanya chochote kufuatia ukosefu wa pesa za kununua kemikali ambazo watatumia.
“Wauzaji wa kemikali wakati huu wameapa kuwa hawatatupatia kemikali bila malipo,”alisema Ochoke.
Aliongeza “Ikiwa serikali haitatuma pesa ifikapo Jumatano, wanafunzi wataandika majina kwenye makatarasi yao ya mtihani na kuziwasilisha kumanisha wataanguka mtihani huo.”
Pia alisema serikali haijawalipa walimu wa kutoa ulinzi katika mitihani hiyo na kuhofia huenda wengi wao wajiondoe.