Vijana nchini wameombwa kujihusisha na sekta ya Jua Kali ili kujiendeleza kimaisha.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Wafanyibiashara Vidogo Vidogo nchini Athony Kwache ambaye alikiri kuwa wengi wamejiendeleza kupitia Jua Kali na biashara vidogo vidogo.
Akiongea mnamo siku ya Ijumamosi mjini Kisii, mwenyekiti huyo alisema sekta ya Jua Kali imesaidia vijana kwa asilimia kubwa nchini na kuomba vijana wengine kujihusisha na sekta hiyo ili kujiendeleza na kuinua uchumi wa taifa.
“Naomba vijana wote nchini hasa wale wa kutoka kwenye kaunti ya Kisii kujihusisha na sekta hii ya juakali kwani ina matunda ya kupendeza ili kujiimarisha kimaisha," alisema Kwache.
Aidha, mwenyekiti huyo aliomba serikali ya kitaifa na zile za kaunti kuungana na kushirikiana kufadhili sekta hiyo ili kuinua sekta hiyo zaidi nchini.
“Changamoto zile sekta ya Jua Kali na wafanyibiashara ndogo ndogo hupitia ni kufanyia biashara zao katika sehemu zisizo nzuri. Naomba serikali kuweka mikakati ya kuwatafutia wafanyibiasara hao sehemu zilizo nzuri na mazingira mema ili uchumi uendelee kuinuka zaidi nchini,” aliongeza Kwache.
Kulingana na mwenyekiti huyo, sekta ya Jua Kali mwaka jana wakati nafasi za ajira zilikuwa zinaundwa nchini iliunda nafasi 6,066 kati ya nafasi 8,000 ambazo ziliundwa nchini na kusema sekta hiyo ndio ilitoa nafasi nyingi na kusema sekta hiyo ya juakali yastahili kuungwa mkono zaidi nchini ili vijana wakuze biashara zao na kuinua uchumi.