Daktari mkuu katika Kaunti ya Nyamira Jack Magara amesema watapeana neti kwa wakazi kwanzia mwezi wa tisa hadi mwezi wa 10 mwaka huu, kama njia moja ya kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria.
Neti hizo zitatolewa kupitia Idara ya Afya katika Kaunti ya Nyamira kwa ushirikiano na chama cha USAID na kile cha Population Service Kenya.
Akizungumza siku ya Jumanne na waandishi wa habari mjini Nyamira, Magara alisema kuwa usajili wa watu tayari umeanza na neti zitatolewa kwa wale wamejiandikisha ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria katika kaunti hiyo.
“Kama Idara ya Afya na washirikishi wetu, tuko na mpango wa kupeana neti kwa wakazi wa kaunti hii na kitengo cha kwanza ni usajili wa watu katika kila sehemu ya kaunti ambao tayari umeanza ili neti zipeanwe,” alisema Magara.
Aliongezea, “Kwa sasa tuna neti zaidi ya 460,000 ambazo wakazi watapokezwa ili mambukizi ya ugojwa wa malaria yapungue.”
Aidha, afisa wa Idara ya afya katika kaunti ya Nyamira Douglas Bosire amewaomba wananchi wote wa kaunti ya Nyamira kuhakikisha kuwa wamejiandikisha ili kupokezwa neti hizo.