Wakulima wa miwa kutoka eneo bunge la Mugirango Kusini wameiomba serikali ya Kaunti ya Kisii kuwatafutia soko la miwa ili kujiimarisha kibiashara.
Wakiongea na Waandishi wa habari siku ya Jumanne katika eneo la Tabaka, wakulima hao walilalamika kuwa hawana soko la kuuza zao lao, hali ambayo wamedai kuwaimesababisha kushuka kwa bei ya miwa ikilinganishwa na hapo mbeleni.
“Mimi nilianza upanzi wa miwa mwaka wa 1998 na ilikuwa na soko nzuri wakati huo, lakini kwa sasa hatuna kamwe soko la miwa na ndio maana sisi wakulima wa miwa kutoka eneo hili la Mugirango kusini tunaomba serikali yetu ya kaunti kututafutia soko ili tuone umuhimu wa ukulima huu,” alihoji Joseck Ontiri, mkulima wa miwa Tabaka.
Wakati uo huo, wakulima hao walisema wamekuwa wakiahidiwa kuwa kiwanda cha miwa kitajengwa katika eneo hilo tangu serikali ya kaunti ya Kisii iingie mamlakani, jambo ambalo wanasema bado hawajaliona likitekelezwa na kushughulikiwa.
“Serikali ya kaunti ilisema itatujenge kiwanda cha kusaga miwa na tumengoja hadi tumechoka maanake muda ndio unaendelea kuyoyoma ndio maana tumelazimika kuiomba serikali ya kaunti itutafutie soko ili tuwe tunauza miwa yetu haraka na kwa faida,” alisema George Obwoge, mkulima mwingine.
Wakulima hao hata hivyo wamesema wana subira ya kutafutiwa soko la miwa waweze kufurahia zao lao maana miwa ndio hutengemewa na wengi katika eneo la Kisii kando na ndizi na parachichi.