Share news tips with us here at Hivisasa

Wanafunzi wa kidato cha nne katika shule zote zilizomo Kaunti ya Nyamira wameonywa kutojihusisha na visa vya wizi wanapoendelea kufanya mitihani yao ya kitaifa inayoendelea kote nchini.

Onyo hilo limetolewa baada ya mshukiwa mmoja kupatikana akiwa na makaratasi ya mtihani huo wa KCSE.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Alhamisi afisini mwake iliyoko mjini Nyamira, afisa wa elimu katika Kaunti ya Nyamira Leo Juma aliomba wanafunzi kutoshiriki udanganyifu wakati wa mitihani hiyo.

Juma alisema kuwa matokeo ya watakaohusishwa na udanganyifu yatafutiliwa mbali kisha wanafunzi hao watalazimika kurejea shuleni au kufeli, jambo ambalo si nzuri kwa mwanafunzi ambaye amekaa darasani kwa miaka minne.

“Naomba kila mwanafunzi aandike kile alifunzwa na walimu pamoja na kile amejisomea mwenyewe. Ukipatikana ukiiba, basi lako haliko maana wizara ya elimu imejitokeza na sheria zingine tofauti, za kukabiliana na watakaoshiriki udanganyifu,” alisema Juma.

Wakati huo huo, afisa huyo alitoa onyo dhidi ya wanaosambaza makaratasi ya mitihani, kwa kusema kuwa watatiwa mbaroni kisha kukabiliwa kisheria.

Aliwahimiza wakazi kutofanya biashara aina hiyo na kutafuta biashara tofauti, badala ya kujiweka katika hatari.