Share news tips with us here at Hivisasa

Bunge la Kaunti ya Uasin Gishu limelaumu afisi ya gavana wa kaunti hiyo kwa kuzembea kutekeleza sheria ambazo bunge hilo limepitisha kwa ajili ya kuafikia malengo ya ugatuzi.

Spika wa bunge hilo Bw Isaac Terer alisema bunge hilo limefanikiwa kupitisha zaidi ya sheria 20 ambapo imekuwa vigumu kwa sheria hizo kutekelezwa vilivyo.

Bw Terer alilaumu maafisa wanaohusika na utekelezaji wa sheria husika kwa kusitasita katika kuweka mikakati ya kuona kwamba sheria hizo zimetekelezwa.

"Sisi kama bunge tumepitisha zaidi ya sheria 20 na miswada 100. Tatizo kubwa ambalo tuko nalo ni kwamba afisi ya gavana imezembea kutekeleza majukumu yake ya kuona kuwa sheria husika zimetekelezwa,” alisema Terer.

Aliongeza, “Iwapo hali hii itaendelea, itakuwa vigumu kwa wananchi kufurahia matunda ya ugatuzi. Kuna njama ya kulemaza shughuli za bunge ili wananchi wafikirie eti bunge limezembea ilihali tunafanya kazi usiku na mchana kwa ajili ya kuafikia malengo ya ugatuzi.”

Msimamo wa Terer uliungwa mkono wa mwakilishi wa Wadi ya Huruma katika bunge hilo Bw Peter Chomba ambaye alitaka afisi ya gavana kuajibika vilivyo ili kuwezesha bunge hilo kutekeleza majukumu yake bila mvutano kati ya taasisi husika.

Bw Chomba alimtaka Gavana Jackson Mandago kuheshimu majukumu ya bunge la kaunti kama njia moja ya kuona kwamba malengo ya ugatuzi yameafikiwa.

Wakati huo huo bw Chomba alilaumu mkuu wa idara ya fedha Bw Shadrack Sambai kwa kuzembea katika majukumu yake.

“Mkuu wa idara ya fedha amezembea katika majukumu yake na hiyo ndio sababu tunataka aondolewe mamlakani.

Akijibu madai hayo kwa niaba ya afisi ya gavana mkurugenzi wa mawasiliano katika afisi ya gavana Bw Cylus Tarus alipinga madai hayo kwa msingi kuwa ni madai ya ubinafsi.