Huku ulimwengu ukiadhimisha siku ya kimataifa ya haki za kibinadamu, shirika la wanawake mawakili FIDA limetoa ripoti inayoonyesha akina baba wengi katika ukanda wa Pwani, wanakwepa majukumu yao katika malezi ya watoto.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika eneo bunge la Changamwe, wakili katika shirika hilo Angela Chege, alisema akina baba wengi hukataa kuwalipia watoto wao karo, huku wengine wakiwadhulumu watoto wao kimapenzi.
“Kwa kila mtoto mmoja kati ya kumi wa kiume na mmoja kati ya watano wakike, wamedhulumiwa kimapenzi katika eneo la Pwani. Lakusikitisha ni kwamba wengi wa wanaotekeleza uhalifu huo hukwepa mkono wa sheria,” alisema Chege.
Chege aliwataka akina baba kuwajibika na kijuhusisha katika malezi ya wanao kwa kuwalinda na kuwa mwelekeo mwema kwao.
Akizungumza katika hafla hiyo, Solomon Madaraka, mzazi wa mtoto aliyenajisiwa alisema kuwa licha ya kupiga ripoti katika kituo cha polisi na hata mshukiwa kuagizwa akae rumande na mahakama, bado anaonekana akizunguka huku asijue lini atapata haki yake.