Mbunge wa Nakuru Mjini Magharibi Samwel Arama amewashauri vinara wa muungano wa Cord Raila Odinga na Kalonzo Musyoka kuvunja vyama vyao na kuunda chama kimoja iwapo wana nia ya kunyakua urais wa taifa.
Akiongea katika hoteli moja mjini Nakuru siku ya Jumatatu, Arama alisema kuwa Raila na Kalonzo watakuwa na nafasi nzuri ya kunyakua uongozi chini ya chama kimoja cha kisiasa.
Aliwataka wawili hao kuweka kando matakwa yao ya kisiasa ya kibnafsi na kuunda chama kimoja kitakacho pambana na chama kipya cha Jubilee.
"Iwapo Raila na Kalonzo wanataka kuliongoza taifa hili, ni sharti waungane ndani ya chama kimoja kwa sababu vyama vingi vinawanyima nafasi ya kushinda uchaguzi. Wanapaswa kuwaunganisha wafuasi wao ndani ya chama kimoja kikubwa kitakachokuwa na sura ya kitaifa," alisema Arama.
Aidha, Arama alimtaka Raila kufanya kila juhudi na kumshawishi kiongozi wa chama cha Amani Musalia Mudavadi kumuunga mkono wakati wa uchaguzi wa mwaka 2017.
Alisema kuwa iwapo Mudavadi atamuunga mkono Raila, hatua hiyo itamwezesha kunyakua urais kwa njia rahisi.
Hata hivyo, mbunge huyo alisema kuwa ataendelea kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta na serikali yake hadi mwaka 2017.