Askari jamii wanaohudumu mjini Mombasa sasa watalazimika kukaguliwa kabla kuruhisiwa kutoa huduma, baada ya kuzuka madai kuwa wana wadhulumu wananchi wasio na hatia.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, naibu kamishna wa kaunti ya Mombasa, Salim Mahmoud, alisema kuwa maafisa hao watafanyiwa ukaguzi ili kubaini utendakazi wao katika hatua inayolenga kuwatema wanaotumia nafasi zao vibaya.
Aidha, Mahmoud alithibitisha kuwa tayari amepokea malalamishi kutoka kwa wananchi wanaodai kuhangaishwa na maafisa hao huku wengine wakidaiwa kuhusika katika visa vya ulaji rushwa mjini humo.
“Tayari nimejulishwa kuwa wapo baadhi ya maafisa wa jamii ambao badala ya kuwahudumia wananchi wanachukua hongo. Tabia hiyo lazima ikomeshwa,” alisema Mahmoud.
Naibu kamishna huyo vilevile amewaonya maafisa hao kuwa yeyote atakayepatikana na hatia ya kushiriki visa vya ufisadi atakabiliwa kwa mujibu wa sheria.
Katika siku za hivi majuzi, wananchi mjini Mombasa wamekua wakilalamika kua baadhi ya maafisa hao hutumia nguvu kupita kiasi, huku wengine wakiwalazimu wenyeji kutoa hongo wanapo patikana na hatia.