Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Walinda usalama katika kivukio cha Ferry Likoni wametakiwa kuwa waangalifu zaidi ili kuzuia usafirishaji wa dawa za kulevya na bidhaa zingine ghushi ikiwa kama njia mmojawapo ya kukabiliana na biashara haramu nchini.

Kauli hii ilitolewa siku ya Jumamosi na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Likoni Willy Simba baada ya mwanamke wa miaka 45 kukamatwa akisafirisha misokoto 350 ya bangi katika kivukio hicho siku ya Jumamosi.

Willy Simba alipongeza ushirikiano baina ya wananchi na askari wa kivukio hicho kwa kushirikiana katika kumtia mbaroni mwanamke huyo.

“Tulipewa habari na mwananchi kuhusu mwanamke huyo kabla ya kueka mtego na kukamatwa na mifuko ya bangi iliyokuwa imechanganywa na samaki aina ya omena," alisema Simba.

Aidha, Bw Simba aliongeza kuwa ameongeza maafisa wa polisi katika kivukio hicho ili kukabiliana na visa kama hivyo.