Share news tips with us here at Hivisasa

Huku matokea ya mitihani ya kitaifa ya KCSE yakitarajiwa kutangazwa hii leo, baraza la mitihani nchini limeombwa kuweka wazi matokeo hayo na kutangaza shule zilizofanya bora pamoja na wanafunzi.

Katibu wa chama cha kutetea maslahi ya walimu nchini KNUT kaunti ya Mombasa Dan Aloo amesema kuwa Baraza la Mitihani ya kitaifa nchini KNEC linafaa kutangaza matokeo ya wanafunzi bora, shule bora kabla ya kuangazia kaunti zilizofanya bora nchini ili kupeana motisha kwa wanafunzi.

Akiongea na wanabahari mjini Mombasa siku ya Jumatano, Aloo alisema kuwa ili kuimarisha viwango vya elimu na sekta ya elimu kwa jumla, kuna umhimu mkubwa iwapo matokeo hayo yataorodheshwa kulingana na jinsi wanafunzi walivyofanya mitihani hiyo kuliko kuorodheshwa katika viwango vya kikaunti.

Aidha alisema kuwa kama viongozi wa chama cha kutetea maslahi ya walimu nchini watahakikisha kuwa mpangilio uliokuwa hapo awali wa kutangaza matokeo ya mitihani ya kitaifa nchini unarejeshwa kwani mfumo uliobuniwa kamwe haujainua viwango vya elimu.

“Tunawaambia maafisa wa baraza la mitihani nchini kuhakikisha kuwa wanatumia mfumo wa awali wa kutangaza matokeo ya mitihani, ndio unaleta msukumo kwa wanafunzi kufanya vyema zaidi darasani na katika mitihani yao, na sisi tunasema kuwa mfumo uliopo sasa bado hatujaridhishwa nao,” alieleza Aloo.

Hata hivyo, matokeo hayo ya mitihani ya kitaifa ya KCSE yanatayarajiwa kutangazwa na Waziri wa elimu nchini Fred Matiangi kisha kuwasilishwa kwa wakuu wa idara ya elimu katika kila kaunti kabla ya kuwasilishwa katika shule za upili.