Huku mvua ikiendelea kunyesha katika maeneo tofauti nchini, wafanyibiashara wa makaa Nakuru wanakila sababu ya kutabasamu kufuatia biashara hiyo kunoga.
Mahitaji ya bidhaa hiyo yameongezeka huku bei yake ikipanda katika mitaa tofauti katika Kaunti ya Nakuru.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatano, wafanyibiashara hao walisema ongezeko la bei ya makaa limesababishwa na kuongezeka kwa baridi inayoletwa na mvua.
“Kuna baridi nyingi sana na makaa huwa yanatumika sana wakati kama huu na ndio maana unaona bei imepanda,” alisema Peter Murugu, muuzaji wa makaa.
Kwa kawaida mkebe wa kilo mbili wa makaa huuzwa kwa Sh25 lakini sasa bei hiyo imepanda hadi kati ya Sh30 na Sh35.
Agnes Mwangi ambaye ni muuzaji wa makaa katika mtaa wa whitehouse alisema kuwa alilazimika kupandisha bei ya makaa baada ya wachuuzi kupandisha bei ya jumla ya makaa.
“Bei ya kila gunia la makaa ilipanda na ikabidi hata sisi wauzaji rejareja tupandishe bei ili tupate faida,” alisema Mwangi.
Kulingana na Andrew Bor ambaye ni mchomaji na muuzaji makaa katika eneo la Rongai, wakati wa mvua huwa vigumu kwao kuchoma makaa na hiyo hupelekea upngufu wa bidhaa hiyo na kusababisha ongezeko la bei.