Wito umetolewa kwa taasisi za kifedha ambazo zilikuwa zimetoa mikopo kwa wafanyibiashara wa soko la Kibuye, Kaunti ya Kisumu, kutoa muda zaidi kwa wateja hao kujiimarisha kabla ya kulipa mikopo hiyo.
Haya yanajiri baada ya soko hilo kuteketea usiku wa siku ya ijumaa, na kuwaacha wafanyibiashara hao wakikadiria hasara ya mamilioni ya pesa.
Akizungumza kuhusu moto huo, Gavana wa Kaunti ya Kisumu Jack Ranguma aliahidi kuzungumza na wakuu wa benki husika pindi atakapopokea orodha ya wafanyibiashara waliochukua mikopo kwenye benki, kuhusiana na pendekezo hilo.
Alisema kuwa mpango wa serikali ya Kaunti ya Kisumu kuimarisha soko la Kibuye kufikia hadhi ya kimataifa utakuwa tayari baada ya mwezi mmoja kuanzia sasa, na shuguli hiyo ya uimarishaji itagharimu shilingi bilioni mbili.
“Takriban shilingi bilioni mbili zitatumika kubadilisha sura ya soko la Kibuye. Licha ya kuwa hatuna pesa hizo kwa sasa, ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa mpango wa kuimarisha soko hili unaafikiwa,” alisema Gavana Ranguma.