Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi katika Kaunti ya Kisii wameshauriwa kutunza mazingira ambayo ni muhimu kwa maisha ya binadamu kwa kupanda miti kwa wingi.

Akizumgumza siku ya Jumanne katika Shule ya Msingi ya Nyambere iliyoko mjini Kisii, wakati wa zoezi ya upanzi wa miti, mke wa Gavana wa Kaunti ya Kisii Bi Elizabeth Ongwae, aliwashauri wakazi wa Kisii kupanda miti kwa wingi na kuitunza bila kuikata kiholela.

Kulingana naye, mazingira hutunzwa kwa kupanda miti kwa wingi kwa kuwa miti huleta hewa safi.

Aidha, Bi Ongwae aliomba wakazi kuasi tabia ya kukata miti kiholela na kuwashauri wanapokata mti mmoja kupanda miti miwili, kama hatua ya kuendelea kutunza mazingira katika Kaunti ya Kisii.

“Naomba wakazi wa kaunti yetu ya Kisii muwe mnatunza mazingira yetu kila wakati ili tuwe na hewa safi. Nawaomba mpande miti kwa wingi na msiwe mnakata miti kiholele,” alisema Bi Ongwae.

Bi Ongwae aliwahimiza wanawake kuwa katika mstari wa mbele katika upanzi wa miti na kuwataka pia kuhakikisha kuwa wanatunza miti hiyo.

Hata hivyo, Bi ongwae aliwaonya wakazi dhidi ya kupanda miti karibu na mito.

Miti 1500 ilipandwa katika shule hiyo huku zoezi hilo likiendelea katika shule zote za kaunti, hospitali na katika afisi za serikali.