Wauzaji nguo na vinyago katika mji wa Nakuru wanachuma pakubwa kutoka kwa wateja wanaonunua mavazi na bidhaa hizo kama matayarisho ya kukaribisha Krisimasi na mwaka mpya.
Kitamaduni, sherehe za Krisimasi huambatana na marembesho ya nyumba, vyakula vya hali ya juu, mavazi mapya, kutembelea marafiki na watu wa familia kati ya mengine.
Hali hiyo imewapa wanabiashara wa nguo maarufu za ‘Mtumba’ faida si haba, huku bei ikiongezeka kutokana na ongezeko la mahitaji.
Kulingana na Simon Kamau muuzaji wa nguo mjini humo, mbeleni alikuwa akiuza nguo moja kwa shilingi mia tano, lakini sasa anauza kwa kati ya shilingi mia nane na elfu moja.
Naye Jacqueline Wanjiku alisema msimu huu wateja hununulia watoto kila iana ya vifaa vya kuwafurahisha.
“Mimi siuzi nguo kwa sababu naamini watoto ndio hununuliwa vitu msimu huu. Nauza bidhaa za watoto kuchezea,” alisema Wanjiku.
Hata hivyo hali ni tofauti na wanabiashara wa vinyago, ambao wanasema ili kuvutia wateja zaidi wa Kiafrika kuliko watalii kutoka nje ya bara Afrika, wamelazimika kuuza bidhaa zilizo na marembesho ya tamaduni za kiafrika.
Wauzaji wa shati pia wameongeza bei kutoka shilingi mia nne, hadi mia saba kwa kadri.