Share news tips with us here at Hivisasa

Bodi ya Utalii nchini imeahidi kushirikiana na serikali kuu, zile za kaunti na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii nchini ili kuhakikisha mikakati mwafaka imeidhinishwa ili kuboresha sekta hiyo.

Kulingana na mkurugenzi mkuu wa bodi hiyo Muriithi Ndegwa, japo sekta hiyo inakumbwa na changamoto, lazima iimarishwa zaidi ili kuwavutia watalii wengi wanaonuia kuzuru taifa hili na kukuza uchumi wa nchi.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, Ndegwa alisema kwamba tayari mikakati ya kuimarisha sekta hiyo imeanzishwa kwani viongozi mbalimbali wa sekta ya utalii ikiwemo Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Biashara na Utalii nchini Bi Phyllis Kandie alichukua jukumu la kuwashauri viongozi wa mataifa ya magharibu kuwaruhusu raia wao kuzuru humu nchini.

Alisema kwamba kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali, sekta ya utalii itaimarika kwa kiwango kikubwa na kurejea hali yake ya hapo awali.

Wakati huo huo Ndegwa alisema kwamba Bodi ya utalii nchini iko na matumaini ya kuwasili kwa watalii wengi zaidi nchini kwani serikali imeweka usalama dhabiti katika kila eneo kuzuia kuhangaishwa kwa watalii pamoja na wananchi wasio kuwa na hatia.

"Kama idara ya utalii nchini, tuko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuona kwamba sekta ya utalii inaimarika kwa kiwango kikubwa na kuwavutia watalii wengi nchini. Serikali imeweka mikakati mwafaka ya kuimarisha usalama kwa hivyo hatuna budi ila kujizatiti na kuimarisha sekta hii,” alisema Ndegwa.

Hatua hiyo imejiri baada ya meli tatu za watalii kutia nanga katika Bandari ya Mombasa kwa kipindi cha miazi mitatu hali ambayo imedhihirisha kuwa sekta hiyo imeanza kuimarika.