Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Bodi zote za shule za msingi na za upili katika kaunti ya Kisii zimeombwa kushirikiana na walimu wa shule kuinua viwango vya masomo katika kaunti hiyo.

Akizungumza siku mnamo siku ya Jumatano katika eneo la Masaba wakati bodi zote za shule zilikuwa na mkutano wa pamoja, mwenyekiti wa elimu katika kaunti ya Kisii Henry Onderi alisema bila ushirikiano kati ya bodi za shule na walimu, viwango vya masomo vitadidimia katika kaunti hiyo.

Onderi aliomba bodi hizo kuwa na ushirikiano mwema na kutafuta suluhu wakati shida inapotokea ili viwango vya masomo kuinuka, na ata kuchukua nambari ya kwanza nchini katika matokeo ya mitihani ya kitaifa.

Kulingana na Onderi, shule inapofanya vibaya, wa kwanza kulahumiwa ni bodi za shule kwa kulala na kutofuatilia jinsi walimu hufanya kazi kila muhula, kisha baadaye walimu kwani masomo ni ya muhimu wakati wanafunzi wanapofanya vizuri.

“Shule inapofanya vibaya, wa kukosolewa ni bodi za shule na walimu, naomba walimu na bodi zenu kushirikiana kutafuta mbinu nzuri itakayowawezesha kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa,” alisema Onderi.

“Tunahitaji kaunti ya Kisii iongoze katika maswala ya elimu nchini, na kuafikia hilo sharti sisi zote tushirikiane pamoja,” aliongeza Onderi.

Aidha, Onderi aliomba walimu kutokubali sherehe za mazisha kufanyiwa katika viwanja vya mashule kwani hafla hizo huchangia kuathirika kwa masomo.