Bunge la Kaunti ya Mombasa limekosolowa kwa kile kilichotajwa kama kupitisha miswada isiyokuwa na manufaa kwa wakazi wa kaunti hiyo, kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu tangu serikali kugatuliwa.
Kiongozi wa vijana katika eneo la Kisauni Maxwell Masai, alidai kuwa miswada iliyojadiliwa katika bunge hilo na kupitishwa imewanufaisha baadhi ya watu fulani walio na ushawishi mkubwa katika kaunti hiyo, bali sio wakazi wa mashinani.
Akizungumza katika mkutano wa vijana huko Kisauni mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Masai alisema kuwa kuna haja ya wakazi wa mashinani kunufaika na miswada hiyo hasa katika masuala ya maendeleo, wala sio kupitishwa kwa miswada isiyokuwa na umuhimu wowote.
"Tunawaomba viongozi wa wadi katika Kaunti ya Mombasa kuhakikisha kuwa miswada wanayoipitisha bungeni inawanufaisha wakaazi. Wakiendelea kupitisha miswada ya kuwanufaisha wao wenyewe na watu wengine wenye ushawishi mkubwa katika kaunti hii basi tutawaondoa mamlakini pindi uchaguzi mkuu utakapofika,” alisema Masai.
Aidha, amewataka wawakilishi wa wadi kuchukua jukumu la kusikiliza matakwa wa wakaazi wa kaunti hiyo kabla ya kuwasilisha hoja katika bunge hilo, ili kaunti hiyo kufanikisha ajenda zake muhimu za kimaendeleo na kukuza uchumi wa kaunti hiyo.
Kauli ya kiongozi huyo wa vijana imejiri baada ya bunge hilo la Kaunti ya Mombasa kupitisha mswada wa kutenga fedha kutoka kwa hazina ya kaunti hiyo kukamilisha miradi iliyokwama.