Share news tips with us here at Hivisasa

Watetezi wa haki za kibinadamu katika Kaunti ya Mombasa pamoja na miungano ya vijana wamelitaja bunge la kaunti hiyo kama lililozembea majukumu yake.

Wakiongozwa na kiongozi wa vijana katika eneo la Kisauni mjini Mombasa Maxwell Masai, watetezi hao wasema kwamba bunge hilo limekuwa likifanya vikao katika mahoteli na kufuja mali ya umma, huku wakisingizia utendakazi bora.

Akizungumza na wanahabari katika eneo la Kisauni mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Masai alisema kwamba hatua iliyochukuliwa na wabunge wa kaunti hiyo haijaweka wazi utumizi wa fedha za umma, huku akisema kwamba serikali ya kaunti hiyo inaongoza kwa ufisadi kutokana na kutowaeleza wananchi jinsi shilingi milioni 697 zilivyopotea.

Masai kwa sasa anataka wabunge wa bunge hilo kuchunguzwa kwa madai ya ufujaji wa pesa, huku akiutaja uzembe wa viongozi wa kaunti hiyo kama utakaodidimiza maendeleo ya kaunti nzima ya Mombasa.

“Wabunge wa kaunti ya Mombasa wameshindwa kuwatendea kazi wananchi na kuchangia ufisadi kwa kufuja mali ya umma, na tuwaambia viongozi wetu wa kaunti kukoma kufuja mali ya wananachi,” alisema Masai.