Zoezi la kuwapa chanjo ya polio watoto wadogo walio chini ya miaka mitano lililoanza siku ya jumamosi katika kaunti ya Nyamira limeonekana kuzaa matunda kwa asilimia kubwa.
Akizungumza na waandishi huyu siku ya jumatatu mjini Nyamira, mmoja wa wahudumu wa afya katika kaunti hiyo Lydia Nyakabi, alisema wakati huu idadi kubwa ya wakazi wameonekana kushirikiana na wahudumu wa afya ambao wanaendelea kutekeleza zoezi hilo kuhakikisha wanao wamepata chanjo.
“Zoezi hili la kuwapa watoto chanjo linaendelea vizuri maana idadi kubwa ya wazazi wameitikia wito na walikuwa tayari kuwawasilisha watoto wao ili wapate chanjo na tunaendelea na shughuli hiyo salama salimini, ” alisema Nyakabi.
Ikumbukwe kuwa afisa wa afya katika kaunti ya Nyamira Douglas Bosire siku ya ijumaa aliwaomba wazazi kutosusia na kujitokeza ili wanao wapate chanjo, jambo ambalo limeonekana kuzaa matunda.
Shughuli hiyo itakamilika alhamisi wiki hii.