Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini CIPK linahofia kuongezeka kwa makundi ya vijana yenye misimamo mikali jijini Mombasa.
Akiwahutubia wanahabari katika afisi za baraza hilo huko Mombasa siku ya Jumanne, Katibu mtendaji wa baraza hilo Sheikh Mohammed Khalifa alilalamikia ongezeko la utovu wa usalama unaosababishwa na vijana hao.
Sheikh Khalifa alisema kulingana na jinamizi la utovu wa usalama linalogubika Kaunti ya Mombasa, wakaazi wa kaunti hiyo wanafaa kushirikiana na idara ya usalama katika kupiga vita makundi hayo.
Khalifa alisema kuwa endapo viongozi wa kidini hawatashirikiana na washikadau katika sekta ya usalama, huenda kaunti ikatekwa na makundi ya vijana yenye misimamo mikali.
Aidha, alisisitiza kuwa viongozi wanaofadhili vijana wenye misimamo mikali wachukuliwe hatua za kisheria ili kukabiliana na changamoto ya utovu wa usalama.