Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Baraza la maimam na wahubiri nchini CIPK limepongeza hatua ya kishujaa ya abiria waislamu waliyojitolea kuokoa mauji ya wenzao wakristo waliyokuwa wameabiri basi la kuelekea mjini Mandera.

Katibu mtendaji wa baraza hilo la CIPK Sheikh Mohamed Khalifa amesema kuwa hatua hiyo iliyochukuliwa na jamaii ya kiislamu kuokoa maisha ya wenzao wakristu inafaa kuchukuliwa kwa uzito kwani hatua hiyo imeonyesha undugu na upendo jamii ya kiislamu inavyojali ndugu zao wakristu.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, Sheikh Khalifa amesema kuwa jamii ya kiislamu kamwe haiungi mkono wanamgambo wa Alshabab na wako katika mstari wa mbele kupiga vita ugaidi na kuhubiri amani.

Khalifa amewataka wakenya wote pasi na kuangalia dini wala ukabila kudumisha amani na umoja miongoni mwa jamii sambamba na kuwa na uiano na utangamano ili kuona kwamba wakenya wanaishi kwa undugu na ushirikiano mkubwa.

"Tunawapongeza ndugu zetu waislamu waliyojitolea kuwakinga ndugu zetu wakristo kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi la alshabab na sisi tunasema kuwa jamii ya kiislamu kamwe haiungi mkono ugaidi wala dini haisemi ugaidi ni halali," alisema Sheikh Khalifa.

Kisa hicho kilichotokea siku ya Jumatatu asubuhi katika eneo la Daba katikati mwa mji wa Kotulo na El-Wak, kilisababisha mauaji ya watu wawili na wengine watatu kujeruhiwa baada ya magaidi hao kufyetua risasi wakitorokea msituni.

Basi hilo lilokuwa na abiria 60 walinusurika kifo baada ya jamii hiyo ya kiislamu kuungana na wenzao wakristo kuokoa maisha yao, hatua ambayo imeungwa mkono na viongozi mbalimbali jinsi abiria hao walivyoonyesha uiano.