Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini CIPK, limeunga mkono msimamo wa Waziri wa Usalama Joseph Nkaiserry, wa kupiga marufuku usambazaji wa picha na video za wanajeshi waliouwawa huko Somalia.
Baraza hilo lilisema kuwa sharti kila Mkenya awape wafu heshima yao, kwa kuwa ni kinyume cha haki na sheria kutumia picha za maafisa hao kwenye mitandao.
Akizungumza na wanahari siku ya Jumanne jijini Mombasa, katibu mtendaji wa baraza hilo Sheikh Mohamed Khalifa alisikitikia mtindo huo miongoni mwa Wakenya, na kutoa wito kwa wale wanaotumia nafasi yao vibaya kukomesha hali hiyo.
Aliwataka Wakenya kuendelea kuwapa moyo wanajeshi wa Kenya wanaopigana usiku na mchana ili kuona kuwa raia wa nchi hii wako salama.
“Si haki hata kidogo kutumia na kusambaza picha za watu waliokufa kwenye mifumo ya mitandaoni. Hakuna dini wala mtu anayeunga vitendo kama hivyo mkono. Sharti tuwape wenzetu heshima na kufariji familia za waliofiwa, kwa sababu wanajeshi hao waliacha familia zao na kuenda Somalia kuhakikishia kuwa tuna usalama nchini,” alisema Khalifa.
Haya yanajiri huku mwanamume mmoja akifikishwa katika mahakama moja katika Kaunti ya Kiambu, akikabiliwa na mashtaka ya kusambaza picha za wanajeshi waliouliwa na magaidi kupitia mtandao wa Whatsapp siku ya Jumanne.