Serikali ya kaunti ya Kisii imeombwa kuhakikisha hakuna mawakala katika masoko yake, hii inatokana na shutuma za kunyanyaswa kwa wafanyibiashara ambao bidhaa zao hununuliwa kwa bei ya chini na kupeleka soko zingine mjini Nairobi zinakouzwa kwa bei ghali kwa faida ya mawakala.
Akizungumza katika soko la Riosiri eneo bunge la Mugirango Kusini, waziri wa kilimo na ufugaji Willy Bett aliomba serikali ya Kisii kuhakikisha wafanyibiashara wa kaunti hiyo wanajiinua kupitia biashara zao kwa kuzuia mawakala ambao huwanyanyasa.
“Naomba serikali ya kaunti kusimama kidete dhidi ya mawakala wanaoingia katika masoko yao kwani imebainika kuwa mawakala hao huwanyanyasa wanabiashara sana,” alisema Bett.
Wakati huo huo, Bett alisema ingawa Wizara ya Kilimo iligatuliwa serikali ya kitaifa itaendelea kutoa msaada kwa wafanyibiashara na wakulima mashinani kuhakikisha uchumi wa taifa na wa kaunti umeinuka.
"Serikali ya kitaifa na zile za kaunti zitashirikiana pamoja kusaidia wafanyibiashara ili kuinua uchumi wa taifa,” aliongeza Bett.